Ulimwengu wa Kiislamu Upaze Sauti Kadhia ya Palestina


Mwishoni mwa juma lililopita, vikosi vya Israel viliwajeruhi Wapalestina zaidi ya 100 waliokuwa wakiandamana kupinga hatua ya Israel kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa makazi mapya kwa raia wake huko mashariki mwa Jerusalem pamoja na ukingo wa magharibi wa mto Jordan.


Waandamanaji hao wa Kipalestina walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya majeshi ya Israel kuwafyatulia risasi za plastiki na kuwaacha wengine katika mateso makali kutokana na kushambuliwa na silaha za gesi ya sumu.


Miongoni mwa waliojeruhiwa ni mpiga picha wa kujitegemea, Nidal Ishtiye ambaye anafanya kazi katika shirika la habari la Uturuki, Anadolu Agency (AA). Nidal amesema alipigwa risasi tatu za plastiki mguuni ambazo zilimjeruhi vibaya wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi.


Kutokana na kadhia hii kujirudia mara kwa mara, tumekuwa tukishuhudia au kusikia kauli mbalimbali kutoka kwa viongozi wa dini ya Kiislamu na serikali, wasomi, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu wakipinga ubabe wa utawala haramu wa Israel wa kuendelea kupora ardhi ya Wapalestina.


Lakini kwa bahati mbaya, kauli hizo zimeshindwa kufua dafu kwa sababu mara zote zimekuwa zikitolewa na mtu au nchi moja moja. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa kauli hizo zinatolewa kwa mafungu.


Pengine kukosekana kwa sera maalum ya kuwalinda na kuwatetea Wapalestina ndiko kunakopelekea jeshi la wazayuni kupata ujasiri na uthubutu wa kupora ardhi ya Wapalestina.


Kwa kiasi fulani, kadhia ya Palestina, ni kama wameachiwa Wapalestina peke yao. Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC) ambao kwa kiasi kikubwa unategemewa kupaza sauti kwenye mgogoro wa Palestina na Israel umekuwa ukifumbia macho tatizo hilo.


Hatua ya serikali ya Israel kuendelea kuikalia kimabavu ardhi tukufu ya Palestina ambayo ndani yake kunapatikana kibla cha kwanza cha Waislamu, yani Masjid al–Aqsa inadhihirisha ongezeko kubwa la fikra za chuki kwa Waislamu wa Palestina.


Ajabu ni kwamba Waislamu wengi duniani hawauoni mgogoro wa Palestina na Israel kama wao; na ni jambo hilo ambalo utawala haramu wa Mazayuni umefanikiwa kuutenga umma wa Kiislamu na mgogoro huo. Jukumu la kuikomboa Palestina linaonekana ni la Wapalestina wenyewe, wakati ukweli ni kwamba jambo hili linawahusu Waislamu wote duniani.


Mazayuni wanapandikiza dhana hii kwa sababu wanajua ni rahisi zaidi wao kupambana na Wapalestina kuliko kupambana na umma wote wa Kiislamu. Tulio wengi hatushughulishwi na madhila yanayowasibu Wapalestina kwa misingi kuwa hakuna tunaloweza kufanya ili kuwasaidia.


Utamsikia mtu akisema: “Tumuachie Mwenyezi Mungu mwenyewe atashughulikia jambo hilo.” Subhanallah! Kwa kuzingatia kwamba Waislamu wote ni ndugu, hatua muhimu zinapaswa kuchukuliwa ili kuwanusuru ndugu zetu wa Palestina.


Kwanza: Tuwafunze watoto historia ya Palestina

Tunapaswa kujielimisha sisi na watoto wetu kuhusu utukufu wa ardhi ya Palestina na msikiti wa al–Aqsa, ambao Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) alikwenda mbinguni akitokea hapo.


Masjid al–Aqsa ndiyo eneo pekee duniani ambalo Mitume wote 124,000 wa Mwenyezi Mungu walikusanyika na kusali nyuma ya kiongozi wao, Nabii Muhammad (rehema na amani ya Allah zimshukie).


Kwa hakika Mitume wengi wa Allah ‘Azza Wajalla’waliishi eneo hili na kuzikwa hapo. Marafiki wa Masjid al–Aqsa wamechapisha vitabu vingi vya watoto vinavyowafundisha kuhusu msikiti huu mtukufu.


Hii ni hazina kubwa kwetu, hivyo tunawashauri Waislamu kununua vitabu hivi na kuviweka ndani ya nyumba zao ili watoto waweze kuvisoma. Nyoyo za watoto wetu zitakapojazwa mapenzi ya ‘Masjid al–Aqsa’, hapana shaka watachukua hatua za ukombozi wa msikiti huu na nchi yote ya Palestina.


Pili: Tuizungumzie Palestina katika darsa zetu

Tuielimishe jamii kwa kuanzisha darsa maalumu za kila wiki kuhusu historia ya Palestina na Masjid al– Aqsa. Hili linaweza kufanyika ndani ya misikiti, kumbi za mikutano, vituo vya kijamii na hata nyumbani kwako.


Tusisubiri wazungumzaji maalumu waje kutuelimisha bali sisi wenyewe tuwe wazungumzaji wa mada hii. Nasema hivyo kwa sababu namna bora ya kujifunza jambo lolote ni kufundisha jambo hilo.


Kama huijui historia ya Palestina, kuna ‘materials’nyingi katika mtandao wa intaneti na vitabu vya Kiislamu vinavyoelezea historia ya mgogoro wa Palestina na Israel. Jambo kubwa la kuzingatia ni vyanzo gani sahihi vya kuchukua taarifa hizo kwenye mitandao.


Tatu: Tuijadili Palestina katika khutba za Ijumaa

Ni vizuri makhatib wa sala ya Ijumaa watoe mada zinazohusiana na kadhia ya Palestina ili jamii ya Waislamu ifahamu kwa kina kuhusu taifa la Palestina, msikiti wa al–Aqsa na ukiukwaji wa utukufu wake unaofanyika sasa.


Nne: Tuizuru Palestina

Kwa wale waliojaaliwa neema ya mali, pangeni safari ya kifamilia ya kuizuru Palestina. Gharama za safari hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na kutembelea Makka na Madina. Yeyote atakayezuru Palestina na kusali hata sala moja katika msikiti wa al–Aqsa atapatwa na hisia za kuikomboa Palestina.


Nasema hivyo kwa sababu, hakuna kiwango chochote cha kusoma, kuangalia televisheni au kusikiliza mihadhara kinachoweza kukupa picha halisi ya hofu ya kuishi chini ya ukaliaji kimabavu, kuliko kushuhudia wewe mwenyewe.


Ukizuru Palestina utashuhudia kwa macho yako udhalilishaji mkubwa ambao Wapalestina wa kawaida wanalazimika kuuvumilia kila uchao kutoka kwa majeshi ya Israel yanayoikalia kimabavu nchi yao.


Kuizuru Palestina na msikiti mtukufu wa al–Aqsa kutayaonesha majeshi ya madhalimu kwamba, licha ya juhudi zao, umma wa Kiislamu bado haujaisahau Palestina, na kwamba juhudi zao za kuwadhalilisha Waislamu hazipiti bila ya kutambuliwa na Waislamu duniani kote.


Iwapo utapata fursa ya kuitembelea Palestina utashuhudia madhila yanayowapata ndugu zetu Waislamu kila siku.


Tano: Tuwaombee Wapalestina

Tusipitishe kipindi chochote cha maombi yetu kwa Allah Ta’ala bila ya kuitaja Palestina. Tukimuomba Allah kwa dhati, hapana shaka ataikomboa Palestina katika namna ambayo Yeye mwenyewe ameichagua, na sisi tutakuwa sehemu ya harakati za kuikomboa Palestina

0 Comments